KIMYAKIMYA, OKWI AUNGANA NA WENZAKE ZANZIBAR
Kiungo mshambuliaji wa kutegemewa wa Simba, Mganda, Emmanuel Okwi, ameshusha presha kwenye timu hiyo baada ya kutua nchini tayari kwa ajili ya mechi ya Nani Mtani Jembe 2 itakayopigwa Jumamosi ya wiki hii.
Katika mechi hiyo, Simba inatarajiwa kuvaana na watani wao wa jadi, Yanga.
Kiungo huyo, hivi karibuni alizua hofu kubwa kwenye timu hiyo baada ya kuchelewa kujiunga na wenzake katika maandalizi kutokana na tabia yake ya kuchelewa mara kwa mara anaporejea nyumbani kwao Uganda.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya uongozi wa timu hiyo, kiungo huyo alitua juzi Jumatatu saa tano usiku akitokea kwao Uganda katika mapumziko na kupokelewa na viongozi wa timu hiyo.
Chanzo hicho kilisema, kiungo huyo alitarajiwa kuelekea Unguja, Zanzibar jana Jumanne kwa ndege kwa ajili ya kuwahi kambi ya pamoja ya kujiandaa na mechi ya Nani Mtani Jembe.
“Okwi ametua tayari usiku wa Jumatatu saa tano, akitokea kwao Uganda alipokwenda kwenye mapumziko baada ya ligi kuu kusimama.
“Mara baada ya kutua hiyo juzi, leo (Jumanne) anatarajiwa kuelekea Zanzibar ilipoweka kambi timu ikijiandaa na mechi ya Nani Mtani Jembe itakayopigwa Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Taifa,” kilisema chanzo hicho.
Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Phiri, alikiri staa huyo kuwasili kambini Zanzibar jana mchana.
“Okwi ametua hapa Zanzibar tayari na leo jioni amefanya mazoezi na wenzake, naamini atatusaidia,” alisema Phiri.
0 comments:
Post a Comment