Kimenuka.............AFUKUZWA KAZI KWA KUSHINDWA KUSIMAMIA UJENZI WA MAABARA HUKO TABORA
MTENDAJI wa Kata ya Kinungu katika Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Velilian Mapalala amefukuzwa kazi kwa tuhuma za kutokaa katika kituo chake cha kazi na kushindwa kusimamia ujenzi wa vyumba vya maabara katika kata hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Elibariki Kingu alisema kuwa ameamua kuchukua uamuzi huo baada ya kwenda katika Kata ya Kinungu na kuambiwa na wananchi kuwa mtendaji huyo ana zaidi ya miezi miwili hafiki katika kituo chake cha kazi.
“Ndugu zangu wajumbe mliohudhuria kikao hiki naomba mniunge mkono kwa maamuzi niliyochukua mimi nilikwenda Kata ya Kinungu kukagua ujenzi wa maabara lakini cha ajabu nilikuta wananchi wakilalamika kuwa mtendaji Mapalala hayuko kituoni kwake kwa zaidi ya miezi miwili,” alisema.
Aidha Kingu alidai kuwa haiwezekani mtumishi wa Serikali akapokea mshahara wa bure pasipo kufanya kazi ya serikali na kushindwa kusikiliza wananchi.
Alisema kinachoshangaza mtendaji huyo amekuwa akishinda mjini akila bata na kuku pamoja na kunywa pombe huku Mkurugenzi na Ofisa Utumishi wakimfumbia macho pasipokuchukua hatua yoyote dhidi yake.
Alisema kutokana na hali hiyo yeye kama Mkuu wa Wilaya ya Igunga hayuko tayari kuwa na watumishi wazembe hivyo amemuagiza Mkurugenzi kumchukulia hatua kali mtendaji huyo.
Sambamba na hayo, Mkuu huyo wa Wilaya ameliagiza Jeshi la Polisi Igunga kumkamata mtendaji Mapalala na kumfungulia mashtaka ya kula mshahara wa serikali pasipo kufanya kazi.
0 comments:
Post a Comment