MBOWE AILIPUA SERIKALI KUHUSU BANDARI BUBU ZILIZOPO NCHINI
Mwenyekiti wa Chacha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amesema kuwa uwepo wa bandari bubu zinazopitisha bidhaa kwa magendo kutoka nje ni miongoni mwa sababu zinazoua viwanda vya sukari hapa nchini.
Amesema kuwa viwanda vya miwa vinapokufa, wanaoumia siyo wenye viwanda bali wakulima wa miwa. Mbowe alisema hayo juzi alipohutubia mamia ya wafuasi wa chama hicho mjini Turiani , Mkoa wa Morogoro katika siku ya kwanza ya ziara yake mkoani humo.
Ziara hiyo ni ya Operesheni Delete CCM (ODC) yenye lengo la kuvihamasisha vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kuiondoa CCM madarakani kuanzia katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
“Katika Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi, kuna bandari bubu katika maeneo mengi. Bidhaa kutoka nje ikiwemo sukari zinaingizwa kwa magendo na kuuzwa kwa bei ya chee. Je, sukari ya Mtibwa itapata soko?” alihoji Mbowe.
Alisema kuwa sababu nyingine za kusuasua kwa viwanda hivyo ni Serikali kutoa vibali vya kuingiza sukari kutoka nje bila kulipia kodi.
“Viwanda vyetu vya sukari vitashindana vipi kwenye soko kama kukiwa na sukari inayoingizwa kwa kusamehewa kodi huku nyingine ikiingizwa kwa magendo? Ni wazi viwanda vitakufa na wakulima kuendelea kuwa maskini,”alisema Mbowe.
Alisema kwamba Serikali haina sera nzuri za kulinda viwanda vya wawekezaji wa ndani na kuwa hali hiyo ikiendelea, maisha ya wakulima yataendelea kuwa magumu.
Mwenyekiti huyo alisema viongozi wa Serikali hata wakiwa bungeni wakihojiwa kuhusu matatizo yanayowakabili wananchi. hawasemi ukweli.
“Bungeni mawaziri hawasemi ukweli wanapojibu maswali kuhusu matatizo ya wananchi. Wengine tunashindwa kuzuia hasira zetu, ndiyo maana tunaona ni bora kwenda kufanya mikutano kwa wananchi,” alisema Mbowe.
Naye Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Morogoro, Suzan Kiwanga aliwataka wananchi wa wilaya hiyo kuhamasishana ili waweze kujiandikisha kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Mbowe azuiwa asimalize mkutano
Katika hali isiyo ya kawaida, wafuasi wa chama hicho walitaka Mbowe aendelee kuhutubia, baada ya saa 12.30 jioni, licha ya sheria kukataza.
Baada ya Mbowe kuwaeleza kwamba muda umeisha na anafunga mkutano, walimjibu kwa pamoja wakisema; “ endelea, endelea.”
Mbowe ambaye alikuwa ameongozana na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu alisema kuwa hawezi kuendelea kwa sababu atakuwa anavunja sheria za nchi, lakini akawaahidi atakwenda siku nyingine kwa ajili ya mkutano.
Wafuasi hao walikubali na kuanza kumsindikiza kwa miguu kutoka katika uwanja huo hadi alipofikia.
0 comments:
Post a Comment