WANAFUNZI WATATU WENYE ULEMAVU WA AKILI WABAKWA NA KUPEWA MIMBA HUKO GEITA
Wanafunzi watatu ambao ni walemavu wa akili wanaosoma Shule Maalumu ya Msingi Mbugani, Halmashauri ya Mji Geita wamekatiza masomo baada ya kubakwa na kupata mimba.
Wanafunzi hao wameacha masomo tangu mwanzoni mwa mwaka huu kwa sababu ya ujauzito, baada ya kubakwa na watu wasiojulikana wakiwa njiani kwenda shule.
Akizungumza ofisini kwake juzi, Mwalimu Mkuu Kitengo cha Wanafunzi Walemavu, Mtawa Blacia Mghamba alisema wanafunzi hao wamefanyiwa vitendo hiyo kutokana na shule hiyo kutokuwa na bweni.
Pia, hali hiyo imesababisha mahudhurio ya wanafunzi hao kuwa hafifu kutokana na baadhi ya familia wanazotoka kushindwa kuwawezesha kuchangia usafiri wa kwenda shule, hivyo wengi hubaki nyumbani.
Alisema shule hiyo ina wafunzi ambao ni walemavu wa akili, uono hafifu na viziwi huku walimu waliopo ni wanane kati yao mwanaume mmoja.
“Baadhi yao hawawezi kuhudhuria masomo kutokana na wazazi wao kuwa na kipato duni, kwa hiyo kupata fedha za kuwaleta kila siku kwa daladala inakuwa ngumu, wazazi wengi wanakata tamaa,” alisema Mtawa Mghamba.
Mwalimu huyo alisema mahudhurio ni asilimia 40 kila siku, kwani shule ina wanafunzi 132 na wanaohudhuria ni 53 kila siku.
Na Salum Maige
0 comments:
Post a Comment