Niyonzima: Jamani mwacheni Jaja

UPEPO umebadilika na sasa mashabiki wa Yanga wanamlaumu straika wao, Genilson Santos ‘Jaja’, kwa kutofanya vizuri dhidi ya Simba, lakini kiungo Haruna Niyonzima amewatuliza kwa kuwataka watulie na wampe muda Mbrazili huyo akisema atakuwa mzuri tu. Awali mashabiki wa Yanga walikuwa na mashaka juu ya uwezo wa Jaja, lakini mioyo yao ilitulia baada ya kufunga mabao mawili dhidi ya Azam FC na kuiwezesha timu yake kushinda mabao 3-0 katika mchezo wa Ngao ya Hisani. Lakini Jumamosi iliyopita dhidi ya Simba, Jaja hakuweza kufanya kitu hadi akafanyiwa mabadiliko zikiwa zimesalia dakika kumi mchezo kumalizika nafasi yake ilipochukuliwa na Hamis Kiiza. Kuhusu hilo, Niyonzima alisema: “Kila mchezaji ana uwezo wake na nafasi anayocheza uwanjani ina utaratibu wa kucheza, haiwezekani wachezaji wote wakacheza aina moja ya soka, sasa wanaomlaumu Jaja lazima wajue anacheza nafasi ipi na majukumu yake ni yapi. “Mimi naona wanamwonea bure na kama wanaipenda Yanga basi wampe muda wa kuwa vizuri na ataisaidia timu kama mwanzo, Jaja ametoka katika ligi yenye mfumo tofauti wa uchezaji na hapa, hivyo anahitaji muda wa kuzoea mazingira zaidi na aina ya uchezaji.” Kuhusu mbio za ubingwa, Niyonzima alisema bado safari ni ndefu, lakini atahakikisha anashirikiana vizuri na wenzake ili Yanga itwae ubingwa walioupoteza kwa Azam FC msimu uliopita. “Hakuna asiyetaka ubingwa Yanga, tumejiuliza mambo mengi baada ya kutoka sare na Simba, wote tunawaza kutwaa ubingwa na ili kutimiza malengo tumejipanga kufanya vizuri katika mechi zetu zote zinazofuata,” alisema Niyonzima. Yanga yenye pointi saba, ipo nafasi ya nne nyuma ya Coastal Union ya Tanga, Jumamosi itacheza na Stand United kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga ambapo Niyonzima alisema: “Hatuwezi kuidharau hata kidogo Stand United kwani nayo ni timu ya ligi kuu. “Mechi zetu nyingi za mikoani zinakuwa kama fainali, hivyo tutapambana kupata pointi tatu muhimu.” source,,mwanaspot
Share on Google Plus

About Rafiki Fm Ludewa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: