Kosa kubwa la Rais (na ni kosa kubwa), ni kule kukubali kushirikishwa kosa, badala ya kuwafukuza wale waliomshauri ashiriki kosa lao. Waziri Mkuu aliposhindwa kupinga hoja ya Utanganyika alipaswa kujiuzulu; lakini aliposhindwa kufanya hivyo, na badala yake akamshauri Rais naye akubali kuwa geugeu, Rais angemfukuza pale pale na kuteua Waziri Mkuu mwingine. Rais hakufanya hivyo; na badala yake Rais naye akakubali kweli kuwa geugeu na kushiriki kosa la washauri wake.
Lakini kosa hilo la Rais, pamoja na ukubwa wake wote, haliwezi kufuta kosa la awali la washauri wake na hoja ya kuwataka wawajibike kwa kosa hilo. Na sasa wanalo kosa la nyongeza Ia kumfikisha Rais katika hali ngumu na ya fedheha; na kuiingiza nchi yetu katika mabishano ya chuki zinazoweza kuigawa. Pengine inafaa niseme kwamba inashangaza na kutisha kidogo kuona kuwa kujiuzulu kwa Waziri ye yote kunafanywa kuwa ni jambo la kuvutana au kubembelezana. Ndugu Ali Hassan Mwinyi aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani katika Serikali ya Muungano. Makosa fulani yalifanyika katika Wizara yake. Hakuwa ameyafanya yeye; yalikuwa yamefanywa na watendaji fulani walio chini ya Wizara yake. Alilazimika kubeba lawama, akajiuzulu. Nadhani kuna wengine waliolazimika kujiuzulu kutokana na mkasa huo huo.
Wala kubadili Waziri Mkuu si jambo la ajabu. Ndugu Rashidi Mfaume Kawawa alikuwa Waziri Mkuu wangu kwa muda mrefu. Hakuwa amefanya kosa lolote; lakini nilitaka kumbadili na kuteua Waziri Mkuu mwingine. Nilimwita, nikamwambia hivyo. Tukakaa pamoja, mimi na yeye, tukashauriana na kukubaliana ni nani anafaa kushika nafasi yake. Nikamteua hayati Edward Moringe Sokoine: Najua kuwa watu wa aina ya Rashidi Kawawa ni adimu sana duniani, hawazaliwi kila siku; lakini hata hivyo ni jambo la kushangaza kidogo kwamba viongozi wetu wa Mageuzi, hata bado hatujafa, wanaona kuwa ni kosa kuwakumbusha kuwa vyeo walivyo navyo ni dhamana. Wanadhani kuwa uwaziri ni usultani: ukisha kuwa sultani utakufa sultani! Nadhani wanakosea.
Nchi hii imewahi kung'oa masultani wa kila aina. Tukianza kuvumilia masultani wa kuchaguliwa tutapanda mbegu ya masultani wa kuzaliwa.
Narudia: kumbadili Waziri, hata Waziri Mkuu, si jambo la ajabu. Anaweza kujiuzulu, anaweza kufukuzwa, na nchi isitikisike. Lakini huwezi kumtikisa Rais wa nchi bila kuitikisa nchi yenyewe. Ni vizuri jambo hili likatamkwa wazi wazi na likaeleweka sawa sawa. Maana watu wengine wananong'ona nong'ona kuwajibika kwa Rais kana kwamba ni jambo la mchezomchezotu. Kulazimika kumchukulia hatua Rais wa nchi ni mkasa na balaa kwa nchi yoyote ile. Ndiyo maana tunatakiwa kuwateua na kuwachagua marais wetu kwa uangalifu mkubwa;
na ndiyo maana wakisha kuchaguliwa, wanatakiwa wajiheshimu na kuwa waangalifu sana. Ni jambo muhimu kabisa, kwa kweli la kufa na kupona, kufanya kila jitihada ili kujenga na kuimarisha utaratibu na mazoea ya kuchagua na kubadili Rais wa Nchi yetu kwa njia ya kupigiwa kura, baada ya Rais anayetoka kumaliza kipindi chake kimoja au viwili kwa mujibu wa Katiba. Utaratibu mwingine wo wote haufai, na ni lazima tufanye kila lililo ndani ya uwezo wetu kuuzuia. Mnapolazimika kuutumia, ni jambo la kufanyaje, si jambo la kurukia.
Katika suala hili Iililotufikisha hapa tulipo, watu wa kuwajibika ni Waziri Mkuu, kwa sababu zilizoelezwa kwa kirefu kabisa; na Katibu Mkuu wa CCM kwa sababu hizo na zaidi, maana yeye ndiye aliyekuwa Kiongozi na Mchochezi wa chini chini wa hoja ya Utanganyika. Waziri Mkuu alisarenda ili wenzake, wakiongozwa au kuchochewa na Katibu Mkuu, wasije wakamwacha katika mataa.
Waheshimiwa wawili hawa walikwisha kuambiwa kuwa watamsaidia Rais wao kama wakijiuzulu. Aliyewaambia ni mimi, kwa niaba ya Rais. Katika kikao cha mwisho nilichofanya na Rais kabla ya kuondoka Dodoma kuelekea Dar es Salaam, nilimwarifu kuwa nimeufikisha ujumbe wake kwa Washauri wake waheshimiwa. Nilimwambia kwa mdomo na kwa maandishi, kwamba nilihisi kuwa viongozi hao watafanya mshikamano wa kukataa kujiuzulu. Kama watafanya hivyo, nilisema, tatizo litakuwa lake. Lakini kwa sababu tatizo halitakuwa lake kama Ali Hassan, bali litakuwa lake kama Rais Mwinyi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mimi kwa upande wangu sitakubali liishie hapo. Na kama nilivyohisi, kweli walifanya mshikamano na mkakati wa kukataa kujiuzulu na Rais akawakubalia! Nimeambiwa kuwa ama wao wenyewe au wajumbe wao, walitoa kwa Rais sababu mbili kubwa "za kukataa kujiuzulu”:
(i) Kwanza, Waziri Mkuu akijiuzulu katika hali hii, na Rais akalazimika kuteua Waziri Mkuu mwingine kwa kufuata Katiba ya sasa, ati Wabunge, hasa wale "55" watakataa kumpa kibali Waziri Mkuu mpya huyo! Wabunge hawa sasa wanatumiwa kama chaka la kufichia madhambi ya kila mila! Mimi katika ujinga wangu nilidhani kuwa tatizo moja la Rais katika uhusiano wake na Wabunge, linatokana na kutokuwa na Waziri Mkuu aliyechaguliwa kwa utaratibu mpya; na akapata kibali cha Wabunge.

Jivunie kuwa mwana ludewa
Share on Google Plus

About Rafiki Fm Ludewa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment