Ludewa FC wameibuka mabingwa wa Bonanza la Michezo lililofanyika tarehe 19 Aprili 2025 katika viwanja vya Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa. Bonanza hilo liliandaliwa na Kituo cha Michezo cha Ludewa Sports Center kwa lengo la kuhamasisha michezo na kuibua vipaji vya vijana wa wilaya ya Ludewa, mkoani Njombe.
Bonanza hilo lilihusisha jumla ya timu nne ambazo ni: Ludewa FC, Luana FC, Worrioz United, na Magereza FC. Timu hizi ziliwakilisha maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo na zilipambana vikali kuwania taji hilo.
Katika mchezo wa fainali uliovuta hisia za mashabiki wengi, Ludewa FC walikutana na wapinzani wao wa jadi, Luana FC. Mechi hiyo ilimalizika kwa ushindi wa mabao 2-1 kwa Ludewa FC, na hivyo kuwaweka kileleni kama mabingwa wa bonanza hilo.
Safari ya Ludewa FC kuelekea fainali ilianza kwa ushindi dhidi ya Worrioz United katika mchezo wa awali wa hatua ya mtoano. Mchezo huo ulimalizika kwa sare na hatimaye Ludewa FC kuibuka na ushindi kupitia mikwaju ya penalti. Katika mchezo mwingine, Luana FC waliiondosha Magereza FC kwa ushindi wa mabao 3-1.
Katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu, Magereza FC waliibuka kidedea kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Worrioz United, na hivyo kujinyakulia nafasi ya tatu kwenye bonanza hilo.
Tukio hili limepokelewa kwa shangwe kubwa na wakazi wa Ludewa, likiwa sehemu ya mkakati wa kukuza michezo ngazi ya jamii, kuhamasisha ushiriki wa vijana, na kukuza vipaji ambavyo vinaweza kufika mbali kitaifa na kimataifa.
Akizungumza wakati wa kufunga bonanza hilo, Mwenyekiti wa Kituo cha Michezo cha Ludewa Sports Center, Ndugu Baraka Haule, aliwapongeza wachezaji wote kwa ushiriki wao wa hali ya juu. Pia alitoa wito kwa wadau mbalimbali wilayani humo kushirikiana kwa karibu katika kuendeleza michezo. Katika hatua ya kuonesha nia hiyo, Ndugu Haule alikabidhi vifaa vya mpira wa miguu na mpira wa wavu kwa Chama cha Mpira Wilaya ya Ludewa.
0 comments:
Post a Comment