SEHEMU YA KWANZA: NI MANCHESTER DERBY NI MOURINHO VS GUARDIOLA.
Na.Chikoti Cico.
Saa 8:30 mchana kwa sasa za Afrika Mashariki hapo siku ya Jumamosi macho na masikio ya wapenzi wa soka duniani yataelekezwa jijini Manchester kufuatilia mtanange wa shoka kati ya Manchester United vs Manchester City.
Ni mchezo ambao unawakutanisha marafiki wa zamani lakini maadui wa sasa, ni Jose Mourinho vs Pep Guardiola, makocha wawili wenye falsafa mbili tofauti lakini wenye nia moja ambayo ni ushindi peke yake. Vikosi vya makocha hawa vimegharimu zaidi ya pauni milioni 670 hivyo ukiachana na mchezo wenyewe ni dhahiri huu ni mchezo unaovikutanisha vilabu vyenye kujua kutumia pesa kwenye gulio la usajili wa nyota mbalimbali.
Huu utakuwa mchezo wa 17 kuwakutanisha Mourinho na Guardiola ambapo katika michezo 16 waliyokutana kabla katika vilabu vitano tofauti Mourinho ameshinda mara tatu, Guardiola akishinda mara saba na wametoka sare mara sita hivyo kitakwimu Guardiola mpaka sasa ni kiboko ya Mourinho.
Ukiachana na takwimu hizo makocha hawa wanabaki kuwa makocha wawili mahiri kabisa ktk ulimwengu wa soka huku kila mmoja akiwa amejikusanyia tuzo na vikombe mbalimbali katika mashindano kadha wa kadha. Pia ukiachana na kwamba hii itakuwa “Manchester Derby” ya 172, huu utakuwa mchezo wa kuionyesha dunia kwa mara nyingine kati ya makocha hawa wawili nani ana “taktiki” bora zaidi kuweza kuipa timu yake ushindi, hii ikiwa ni sifa kubwa kila mara Mourinho na Guardiola wanapokutana.
Baada ya michezo mitatu ya ligi ya primia ambayo United na City wameshinda na kujikusanyia alama 9, huu utakuwa ni kama mchezo mwingine wa kufungua pazia la ligi hiyo ni kama kusema sasa ligi ndiyo inaanza ndani ya jiji la Manchester kutokana na uzito wa mchezo wenyewe na makocha husika.
Mpaka sasa Mourinho anayo picha iliyopigwa mwaka 1997 baada ya mchezo wa fainali ya “European Cup Winners Cup” kati ya Barcelona vs PSG wakati huo Mourinho akiwa sehemu ya benchi la ufundi la Barcelona chini ya Bobby Robson na Guardiola akiwa kiungo wa klabu hiyo.
Picha hiyo inawaonyesha Mourinho na Guardiola wakiwa wamekumbatiana kwa furaha, ni ngumu kufikiria kama makocha hawa wawili ambao kwa sasa ni kama chuma na kutu wanaweza kuwa waliwahi kukumbatiana, urafiki wako uliokuwepo kabla kitambo ulifikia tamati toka Guardiola alipopewa kuifundisha Barcelona nafasi ambayo Mourinho ndiye aliyekuwa akipigiwa chapuo.
Kuelekea “Manchester Derby” maneno ya Zlatan Ibrahimovic moja ya wachezaji ambae anawafahamu vyema makocha hawa wawili yanaweza kutoa picha ya namna makocha hawa walivyo, kwa maneno yake mwenyewe akiwa anawaelezea makocha hawa Zlatan amewahi kusema “Kama Mourinho analeta mwanga ndani basi Guardiola yeye hushusha mapazia kuleta giza”
.
SEHEMU YA PILI. NI MANCHESTER DERBY, NI MOURINHO VS GUARDIOLA.
Timu zote mbili za jiji la Manchester zimeshaweka kibindoni alama tisa toka pazia la ligi ya Uingereza kufunguliwa, huku United wakifunga magoli sita na kufungwa goli moja nao City wakifunga magoli tisa na kufungwa magoli matatu.
Kwa namba hizo “hafifu” za magoli ya kufunga na kufungwa kwenye michezo mitatu ya ligi ya primia unaweza kusema mpaka sasa United wana UKUTA mzuri zaidi kuliko City, wakati wao City wakionekana kuwa na safu nzuri ya USHAMBULIAJI kuliko United. Kuelekea mchezo huo kuna maeneo mbalimbali ambayo yanaweza kuamua mbabe wa “dabi” hii kuanzia eneo la ulinzi mpaka eneo la ushambuliaji ukiachana na sababu zingine za nje ya uwanja kama vile United kuwa wenyeji.
WACHEZAJI WA KUCHUNGWA ZAIDI.
Zlatan Ibrahimovic- Akiwa na hamu ya kutaka kumwonyesha Guardiola kwamba alikosea kumpeleka kwa mkopo na kumuuza mwaka 2010 wakati akiwa Barcelona. Ibra ni mchezaji wa kuchungwa sana hasa ukizingatia kwamba mpaka sasa katika michezo mitatu ya ligi tayari ameshafunga magoli matatu.
Akiwa na umri wa miaka 34 bado ameonyesha anayo njaa ya mafanikio chini ya kocha ambaye ni kipenzi chake Jose Mourinho na hivyo City wanatakiwa kufanya kazi ya ziada kumzuia mshambuliaji huyu, ni moja ya wachezaji ambao wanaweza kuamua matokeo ya Manchester dabi. Wayne Rooney- Pamoja na kwamba nahodha huyu wa United anaonekana kupwaya tokea kuanza kwa ligi ya primia msimu huu lakini bado huwezi kumchukulia kawaida Rooney ukizingatia kwamba amezitikisa nyavu za City mara 11 katika michezo mbalimbali aliyocheza dhidi yao.
Na pia katika mechi kama hizi ambazo unaweza kuziita “mechi kubwa” wachezaji aina ya Rooney yaani wachezaji “wakubwa” na wenye uzoefu huwa ndiyo huamka kuleta utofauti na hata kuamua matokeo hivyo Rooney pia anatakiwa kuangalia kwa jicho la tahadhari. Raheem Sterling- Kama kuna mchezaji ambaye ndani ya mwezi mmoja amefanya Guardiola apewe mshahara wake bila maswali basi ni huyu, Sterling ambaye alikuwa anafifia wakati msimu uliopita unafikia tamati amefufuka tena chini ya kocha huyu mpya, beki za United zinatakiwa kukaa sawasawa kumzuia huyu winga machachari.
David Silva- Kiungo huyu mpole mwenye mguu wa kushoto wa dhahabu ndiye hasa injini ya Guardiola katika kuamua mpira uende wapi na kwa wakati gani, chini ya kocha mpya Silva amekuwa akikava eneo kubwa la uwanja huku akiwa na jukumu la kuchukua mpira kutoka kila pembe ya uwanja na kuanzisha mashambulizi huku akitafuta mashimo ya kupiga pasi za mwisho.
Viungo wa Manchester United kwenye eneo la katikati hasa Fellaini watakuwa na kazi kubwa kumzuia mchezaji huyu, kama wakimpa nafasi ya kutawala eneo hilo basi Manchester dabi itaamuliwa na Silva. Huku Bailly kule Stones, wote wana umri wa miaka 22 lakini mpaka sasa ni mabeki ambao makocha wa timu zote mbili wanawategemea katika kuzifanya ngome zao kuwa salama lakini zaidi sana kuleta utulivu kwenye timu zao kutokea eneo la nyuma.
Bailly pia atakuwa na kazi kubwa ya kupambana na yeyote kati ya Nolito ama Sterling ambao mmoja kati yao anaweza kucheza kama mshambuliaji wa katikati baada ya Aguero kusimamishwa na huku Stones akiwa na jukumu zito dhidi ya Ibrahimovic jukumu ambalo linaweza kuamua nani ataibuka mbabe kati ya timu hizi mbili.
Kwa ujumla Manchester Dabi ya msimu huu inaweza kuwa ndiyo dabi itakayokuwa na msisimko zaidi mbele ya mashabiki wa klabu zote mbili na wapenzi wa soka duniani kote na kama itaweza kufikia kilele cha juu kabisa cha ubora na ushindani inawezekana kwa miaka ambayo Mourinho na Guardiola watakuwa ndani ya ligi ya primia basi Uingereza wakawa wamejipatia “EL CLASICO” yao.
Ludewa yetu na maendeleo yetu posted by barnabas njenjema, kutoka Ludewa
0 comments:
Post a Comment