BEKI Nassor Masoud ‘Chollo’ amekosa penalti dakika ya mwisho, Simba SC ikilala 2-1 mbele ya Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Chollo alipiga penalti hiyo ikagonga mwamba wa juu dakika ya 90+3 baada ya beki Yussuf Abdallah kumchezea rafu kiungo Jonas Mkude kwenye boksi.
Chollo alifanya kosa hilo, Simba SC ikitoka kufungwa bao la pili kwa penalti pia na Yussuf Abdallah baada ya kipa Peter Manyika kumshika miguu Raphael Daudi dakika ya pili 90+2.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Abdallah Kambua wa Shinyanga aliyesaidiwa na Anold Bugado wa Singida na Yahya Ali wa Mara, hadi mapumziko tayari Simba SC walikuwa mbele kwa bao 1-0.
Bao hilo lilifungwa na mshambuliaji chipukizi, Ibrahim Salum Hajib dakika ya 45+2 kwa shuti la mpira wa adhabu kutoka umbali wa mita 20, baada ya kiungo Awadh Juma kuchezewa rafu.
Mbeya City ilisawazisha bao hilo kupitia kwa Hamad Kibopile dakika ya 77 akitumia vizuri makosa ya mabeki wa Simba SC kuchanganyana na kipa wao, Peter Manyika.
Simba SC walicheza vizuri kipindi cha kwanza na hata hata kipindi cha pili walikianza vizuri, lakini baadaye wakawapa nafasi ya Mbeya City kuuteka mchezo.
Hiki ni kipigo cha kwanza kwa Simba SC katika Ligi Kuu chini ya kocha mpya, Mserbia Goran Kopunovic aliyeshinda mechi moja 2-0 dhidi ya Ndanda na baadaye sare ya 1-1 Azam FC.
Matokeo hayo, yanaiacha Simba SC na pointi zake 13 za mechi 11, wakati Mbeya City inafikisha pointi 15 za mechi 11.
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment