Kafulila: Sina ugomvi na Werema.

Mwandishi Wetu MBUNGE wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), amesema hana ugomvi wowote na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema. Bali yeye msimamo wake ulikuwa ni kwenye kutetea maslahi ya Taifa na ndiyo maana, alisimama kidete bungeni kuhakikisha wote ambao wamehusika katika sakata la Tegeta Escrow wanachukuliwa hatua. Wakati wa mjadala wa Escrow umepamba moto bungeni, Kafulila kwa sehemu kubwa alikuwa akirushiana maneno na Jaji Werema, ambapo mbunge huyo akaitwa tumbili. Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Kafulila alisema hana ugomvi na mtu yeyote, akiwemo Jaji Werema na kwamba, alikuwa akisimamia maslahi ya taifa, kazi ambayo ameifanya hadi dakika ya mwisho na Bunge kufikia uamuzi wa kutoa maazimio nane kwa Serikali ili kuwawajibisha wanaohusishwa na sakata hilo. Kafulila aliyekuwa akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, alisisitiza kuwa, alichokuwa akikifanya ndani na nje ya Bunge ni kusimamia hoja hiyo kwasababu ilikuwa ya ukweli, hivyo hakuogopa mtu wala cheo, bali alisimama kwenye kupigania haki ya Watanzania. “Nitumie nafasi hiyo kusisitiza, sina ugomvi na Werema. Simchukii na wala sina sababu ya kufanya hivyo, bali kilichotokea nilikuwa nasimamia maslahi ya taifa na si vinginevyo,” alisema Kafulila. Alifafanua kuwa, msingi wa hoja yake ilikuwa ni kuhakikisha sakata la Escrow linazungumzwa kwa uwazi na hakuwa akifanya hivyo kwasababu ya kumchukia Jaji Werema au kiongozi mwingine yoyote. Aliongeza, juhudi zake za kusimamia sakata hilo, ndizo zilizosababisha kujenga tofauti baina yao na linalomfurahisha ni kuona waliohusika wamebainika. “Wakati naanza kulizungumzia jambo hili sikuwahi kufikiria kuwa, najenga ugomvi na mtu, ila niliangalia suala la maslahi ya taifa jambo ambalo limetimia kwa kiasi fulani,” alisema. Aliongeza, alichokuwa akitaka ni kuona uwajibika kwa kila aliyehusika na katu hakuwa anafikiria kujenga chuki na kigogo yoyote.”Ninachotaka ni kuona fedha zinarudishwa na waliohusika wanachukuliwa hatua.” . Wakati huo huo, Kafulila alisema anaungana na kauli za viongozi wa dini ambazo wamezitoa kwenye ibada ya Krismasi na kwamba, walichokifanya ni kutimiza wajibu wao. Pia, alisema sakata la Escrow limesababisha miradi mingi ya maendeleo kukwama. @jambo leo.
Share on Google Plus

About Rafiki Fm Ludewa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: