KEISSY AWAVURUGA TENA WABUNGE WA ZANZIBAR... VURUGU ZAIBUKA, NAIBU SPIKA AOKOA JAHAZI
Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, jana alifanikiwa kudhibiti kuchafuka hali ya hewa bungeni baada ya wabunge kutoka Zanzibar kutaka kumpiga Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Keissy, (pichani) wakichukizwa na kauli yake waliyoitafsiri kuwa ni ya kuikejeli Zanzibar.
Keissy, ambaye mara kwa mara amekuwa akijikuta akiingia katika msuguano na wabunge kutoka Zanzibar, alitoa kauli hiyo akipinga kauli ya Mbunge wa Viti Maalum (CUF), Rukia Kassim Ahmed, aliyoitafsiri kuwa ni ya kukejeli hatua ya Rais Jakaya Kikwete kwenda kutibiwa Marekani.
Rukia alitoa kauli hiyo katika mwongozo wa spika aliouomba bungeni jana chini ya kanuni ya Bunge ya 47 (1), (2) na (3).
Alisema kutokana na serikali kudaiwa na Bohari ya Dawa (MSD) Sh. bilioni 102, hali imekuwa mbaya katika hospitali nchini, wagonjwa wanateseka, dawa hakuna, huku wabunge wakiendelea kupulizwa na viyoyozi bungeni na Rais Kikwete akiwa nje ya nchi kuchunguzwa afya yake.
“Kutokana na Serikali kudaiwa bilioni 102 na bohari ya madawa MSD hali ya Hospitali zetu ni mbaya sana.. wagonjwa wanaendelea kuteseka na maradhi, madawa hamna.. wanawake wanakufa, watoto wanateseka.. huku sisi waheshimiwa wabunge tukiendelea kukaa humu tukila viyoyozi
"Kwa taarifa tulizonazo Mheshimiwa Rais yupo nje kaenda kuchekiwa afya yake.. Ili tuwatendee haki Watanzania waliotuweka katika bunge hili na tuweze kuokoa maisha yao naomba bunge lako liahirishe shughuli zinazoendelea tuweze kujadii jambo hili kwanza.. tulipatie ufumbuzi kwa maslahi ya Watanzania.. na kwa maana hiyo naomba kutoa hoja na waheshimiwa wabunge naomba mniunge mkono..”-Rukia
Baada ya mwongozo huo wa Rukia , Keissy, alisimama na kusema Rukia hakupaswa kulinganisha hoja yake na Rais Kikwete kuwapo nje ya nchi kupatiwa matibabu na kuhoji kama alistahili kwenda kutibiwa Zanzibar.
Keissy alisema anawajua baadhi ya wabunge wa CUF, ambao wamekuwa wakienda mara kwa mara India kutibiwa na kusema iweje Rukia azungumzie habari za Rais Kikwete kwenda kutibiwa Marekani.
“..Wabunge wangapi wa upinzani tayari wameshawahi kwenda India mara sita.. Kwa majina nawajua tena wa CUF wamekwenda India kutibiwa mara tatu mara nne leo mnazungumzia habari ya Rais kwenda kutibiwa Marekani, aende kutibiwa wapi Zanzibar? Acheni mambo yenu hayo.!.”-Kessy
Kauli ya Keissy iliwafanya wabunge kutoka Zanzibar kuhamaki na kuinuka na kutaka kumpiga. Hata hivyo, Ndugai alisimama na kuwasihi watulie na kuepuka kutoa kauli zinazoweza kuchafua hali ya hewa bungeni.
“..Waheshimiwa wabunge ningewaomba sana kuhusiana na masuala ya wagonjwa wetu mbalimbali wawe ni wabunge.. Awe ni mheshimiwa Rais na wanatibiwa wapi.. Naliomba jambo hili tuliache litatuharibia hali ya hewa bila sababu jamani.. Nawaombeni sana hilo nimelitoa katika utaratibu na kwenye hansard tulifute jamani..”-Job Ndugai
Wakati Ndugai akiendelea kuongea, Keissy alisimama na kuondoka katika ukumbi wa Bunge. Baadhi ya wabunge kutoka Zanzibar walimfuata Keissy, lakini wakashindwa kumfikia kutokana na kusindikizwa na askari wa Bunge
0 comments:
Post a Comment