Wednesday, January 28, 2015

MTOTO WA MWEZI MMOJA APIGWA MCHI KICHWANI NA BABA YAKE MZAZI

Sifa Lubasi kutoka Mpwapwa anaripoti kuwa mtoto mwenye umri wa mwaka moja na miezi minne, amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma akiwa na hali mbaya baada ya kupigwa na mchi kichwani na baba yake mzazi. Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Saidi Mawji alisema mtoto huyo, Yadiko Chigoda amepata jeraha kichwani na sasa anaendelea kupatiwa matibabu na uchunguzi zaidi. “Ni kweli tumempokea mtoto huyo akiwa na mama yake na ndugu zake wengine waliomsindikiza, ameumia sana kichwani lakini bado anaendelea na tiba na uchunguzi zaidi kwenye fuvu la kichwa maana inaonesha kama limepasuka,” alisema. Pia, Dk Mawji alisema wanafanya mpango wa kumhamishia mtoto huyo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kwa matibabu zaidi. Akizungumza katika wodi namba saba katika hospitali hiyo, mama mzazi wa mtoto huyo, Caroline Mnyawami (32) ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Mingui Kata ya Lumuma, alisema siku ya tukio majira ya saa nne mume wake, Fabian Chigoda alikuwa akimpiga kaka yake na ndipo akajaribu kuamulia ugomvi huo. Alidai alipojaribu kumnyang’anya mumewe fimbo, aliyokuwa akimpigia kaka yake, ndipo mumewe aliamua kuchukua mchi wa kinu na kumrushia kichwani, ambapo alikwepa na kisha mchi huo kumgonga mtoto, aliyekuwa amembeba mgongoni. Baada ya mwanaume huyo kuona amempiga mtoto, aliamua kukimbia na mpaka sasa hajulikani alipo. Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mingui, Mwingwa Udoba, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema chanzo cha ugomvi ni masuala ya kifamilia. “Bado tunaendelea kumtafuta, kwani alikimbia baada ya tukio na akipatikana atafikishwa kwenye mikono ya sheria,” alisema

No comments:

Post a Comment