Katika hali isiyokuwa ya kawaida Mtendaji wa Kata ya Kakubilo Wilaya ya Geita Mkoani Geita Zefania Chenge amemwapisha mwenyekiti wa kitongoji cha Ikigijo Kijiji cha Kikwete Balele Ngulu wa (CCM), kuwa mwenyekiti wa kitongoji hicho bila kuchaguliwa na wananchi.
Zefania alimwapisha mwenyekiti huyo ambaye hakuchaguliwa na wananchi kupitia kikao cha kamati tendaji ya kijiji cha Kikwete kilichofanyika Januari 23 mwaka huu.
Ngulu alisimikwa kuwa mwenyekiti wa kitongiji hicho baada ya kuahirishwa kwa uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Disemba 14 mwaka jana, kutokana na kucheleweshwa kwa fomu za wagombea wa uenyekiti kutoka CHADEMA na CCM na hivyo kutakiwa kusubiri baada ya siku 90 kwa mujibu wa sheria za uchaguzi.
Kufuatia hali hiyo Viongozi wa Kata ya Kakubilo (UKAWA) waliiomba serikali itengue mara moja uamuzi huo vinginevyo wanaandaa maandamano yasiyokuwa na kikomo katika kata hiyo.
“Sisi kama viongozi wa Ukawa tunamuomba mkurugenzi atengue huu uamuzi wa kuapishwa kwa mwenyekiti huyu sisi pamoja na wananchi hatumtambui na tutaandamana kwa ajili ya hili”,alisema Abdallah Machimu ambaye ni katibu wa Ukawa kata ya Kakubilo.
Kwa upande wa wananchi wa kitongoji hicho walimkataa mwenyekiti huyo na kudai kuwa wao hawamtambui.
“Mwenyekiti huyu aliyeapishwa na Mtendaji sisi hatumtaki kwa sababu hatukumchagua na wala uchaguzi haukufanyika katika kitongoji chetu, sasa huyu bwana wamemtoa wapi mbona tunafanyiwa mambo ya ajabu au kwa vile ni kijijini wanatufanya sisi wajinga? Tunasema hatumtaki,’’walisema wananchi hao.
Malunde1 blog ilimtafuta mtendaji huyo kutaka kujua tuhuma hizo ni za kweli ama ala, simu yake ya kiganjani iliita bila kupokelewa na badaaye kuzimwa.
Hivi karibuni Chenge alituhumiwa na wananchi wa kijiji cha Kabayole kuhusika katika ubadhirifu wa fedha za mradi wa chumba kimoja cha Darasa katika shule ya msingi Kabayole baada ya kujenga darasa chini ya kiwango hivyo kulidanganya baraza la madiwani la mwaka 2014 kuwa boma limekamilika wakati ni uongo.
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment